“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.”
Mwanzo 1:27
Katika jambo la awali kabisa mwanamke kulifanya ni kujitambua. Wanawake wengi wameishi wakiwa hawajioni wao kuwa watu wa maana, imefika hatua ambayo wameanza kujishindanisha na wanaume. Wanapambana ili wajionyeshe kuwa wao ni bora tena ni bora sana kuliko wanaume. Ukishaanza kuona unapambana kushindana na mwanaume ujue shetani ameshakuweza. Mungu alipokuumba mwanamke alikuumba akiwa na kusudi na wewe, angetaka uzaliwe mwanaume asingeshindwa; ile kuzaliwa tu mwanamke kuna kazi amekuamini kwamba ni wewe utaifanya na sio mwanaume kwasababu hiyo kitendo cha kuanza kujifananisha na kujishindanisha na mwanaume ni ishara tosha haujui kwa nini umeumbwa mwanamke. Neno la Mungu lipowazi kabisa kwamba ‘Kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba’ sio mwanaume pekee aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hata sisi wanawake tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Ni fahari iliyoje kujua kuwa hata sisi wanawake ni sura na mfano wa Mungu. Tumeumbwa na kuitwa Adamu, sisi wote wanaume na wanawake ni binadamu hakuna sababu ya kujiona duni. Hata kubarikiwa hakubarikiwa mwanaume tu bali hata sisi wanawake ni wabarikiwa, Mungu alitubariki wote kwa pamoja. Neno la Mungu linasema “Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya; mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa.” - Mwanzo 5:1-2. Biblia inasema mwanamume na mwanamke aliwaumba akawabarikia, hakumbariki mmoja na kumuacha mwingine bali aliwabarikia kwa pamoja wote wana baraka za Mungu, kinachofurahisha zaidi ni Biblia inasema ‘akawaita jina lao Adamu’ hata jina tukaitwa Adamu, jina Hawa lilikuja baadaye kwasababu ya kazi ya uzao na hilo jina mwanamke alipewa na Adamu “Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.” - Mwanzo 3:20. Mpaka sasa unaweza kuwa umeshaanza kuelewa kuwa ni uongo wa shetani wa kufanya wanawake wasijikubali na kujiona watu duni.
UMEUMBWA KWA NAMNA YA AJABU.
Jambo lingine ambalo limekuwa likisumbua wanawake wengi ni kutojikumbali muonekano wao, kitu ambacho kimepelekea kukosa kujiamini na kupoteza kufanya kile Mungu ameweka ndani yetu. Hii imepelekea wanawake kuhangaika sana na muonekano wa nje na kusahau kabisa kushughulika na mtu wa ndani. Sisemi kuhangaika na mtu wa nje ni jambo baya lakini hakikisha haichukui nafasi ya kuhangaika na mtu wako ndani. Mfano kupata muda wa maombi, kuhudhuria ibada, kusoma Neno la Mungu nk ni mambo ambayo yanamjenga na kumnawirisha mtu wa ndani. Pamoja na hayo wewe ni mzuri kwa namna ulivyoumbwa, iwe ni kimo mrefu au mfupi, iwe ni mnene au mwembamba, mweusi au mweupe kuna upekee na uzuri unao ambao hakuna mwanamke au mwanadamu mwingine anao. Wewe ni wa pekee kwenye kila kitu, shetani hutudanganya kuona hatufai nah ii huanza na kutusababishia katika kujifananisha na kujiringanisha na wengine. Mtunga Zaburi anaandika anasema “Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu. Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana,” – Zaburi 139:13-
14. Mungu ametuumba kwa jinsi ya ‘ajabu na kutisha’ mwandishi wa zaburi hii anasema wazi kwamba ninakushukuru kwa kuwa nimeumbwa. Hivi ushawahi kumshukuru Mungu kwa kukuumba? Au ndio umeamini uongo wa shetani wa kukuonesha kuwa wewe ni mbaya, kwamba watu wanakuchukia sababu ya muonekano wako! Sio kweli wewe ni matokeo ya uumbaji wa Mungu wa ajabu na kutisha.
Hauna sababu ya kujichubua ngozi yako, hauna sababu ya kuvaa kiajabu au ki aibu. Biblia inaendelea kusema “Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.” - Zaburi 139:15-16. Kile kitendo umetoka tumboni mwa mama yako, ni matokeo ya Mungu kukuunga tangu ukingali tumboni, ustadi ulitumika lakini kinachofurahisha ni kwamba Mungu hakukuumba tu bali macho yake yalikuona kabla hujakamilika na akaziandika siku zako za kuishi kabla hazijawa bado. Unachopaswa kufanya ni kutambua wewe sio bahati mbaya, na upo hivyo ulivyo kwasababu kuna kusudi Mungu ameweka ndani yako. Wewe ni wa pekee, acha kuhangaika na uongo wa shetani. Usiwe kama Yeremia alisema kuwa yeye ni mtoto, wakati Mungu alimuweka kuwa nabii kabla hata hajazaliwa. “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto.” – Yeremia 1:5-6. Mungu alijua kuwa Yeremia ni mtoto kama ambavyo anajua umbo lako lilivyo. Ila yeye haendeshwi na muonekano unaokusumbua bali anaendeshwa na kusudi lake aliloliweka ndani yako na hilo ndio wewe. Mwanamke jikubali, jipende na ujijali hivyo ulivyo kuna kazi nzuri Mungu ameweka ndani yako anataka uifanye na kuwa faida sio kwa familia yako na uzao wako tu bali uwe baraka kwa mataifa. Wala usijilinganishe na mtu mwingine kwa habari ya baraka wala usijisikie vibaya wengine wanapobarikiwa. Kila mmoja anawakati wake wa kujiliwa, wakati wako wa kubarikiwa upo njiani. Kumbuka Mungu amekuchora katika kitanga cha mkono wake kama anavyosema “Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.” - Isaya 49:17. Huna sababu ya kutembea umeinama, mwamini Mungu anakubariki na kukufanya baraka kwa wengine.
MWANAMKE KAMA MSAIDIZI.
Wanawake wengi hufikiri ile mwanamke kuitwa msaidizi inamaanisha yeye ni mtu duni, kwamba mwanaume anakuwa na thamani kubwa kuliko wao. Sio kweli, kuitwa msaidizi ni zao la mgawanyo wa kimajukumu ambao Mungu ameuweka yeye mwenyewe kwa mapenzi yake lakini kwa ajili yetu ili tuweze kufurahiana. Embu waza dunia yote ingekuwa ni wanaume tu, au dunia yote ingekuwa na wanawake peke yetu. Hakika isingevutia, wanaume na wanawake ndio wanaifanya dunia. Biblia inasema “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” – Mwanzo 2:18. Mungu anasema wazi kuwa msaidizi wa kufanana naye. Kwamba naye atakuwa ni mtu, naye ni mbarikiwa, naye lazima awe sura na mfano wa Mungu naye atatawala samaki wa majini, ndege wa angani, wanyama wa mwituni nk. Ukiviondoa hivyo anakuwa hajafanana na Adamu. Kuna wakati msaidizi anatakiwa kuwa na nguvu kuliko msaidiwa hivyo kuwa msaidizi haimaanishi kuwa mtu duni au kuwa wewe sio bora.
Kwa asili Mungu amemuumba mwanaume kuongoza familia. Kama umekuwa mdau wa mambo ya uongozi utakubaliana na mimi taasisi haiwezi kuongozwa na viongozi wawili lazima kuwe na kiongozi mmoja wengine watamsaidia hata kama wanaitwa viongozi. Nchi haiwezi kuwa na Rais wawili lazima itakuwa na Rais mmoja wengine watamsaidia. Ndivyo namna Mungu ameiweka ndoa kwamba Mwanaume atakuwa kiongozi na mwanamke atamsaidia. Kuna ndoa nyingi zinayumba na nyingine zimevunjika kwasababu tu mwanamke anapambana kuwa kiongozi kwa mume wake na kuiacha nafasi ya asili ya msaidizi ambayo Mungu aliiweka ndani yake. Mungu akupe neema kuifanya kazi yako kwa usahihi na ubora, kuna wakati shetani anataka kukutoa katika nafasi yako kwasababu ya vitu unavyopitia. Ila neema ya Mungu inakutosha kuhakikisha upo salama kwenye nafasi yako.
MWANAMKE NA KUZAA
Pamoja na kuwa msaidizi kuna mambo Mungu ameyaweka ndani ya mwanamke pekee na mwanaume hanayo, na kuna mambo Mungu ameyaweka kwa mwanaume peke yake mwanamke hana. Sasa ni muhimu kuyachochea na kuyatumia vyema yale yote ambayo Mungu ameweka ndani yako na kukufanya uwe wa pekee. Mungu amempa mwanamke tumbo la uzazi ambalo mwanaume hana. Mwanamke amepewa nguvu ya kuongeza, nguvu ya kuzidisha. Wewe ni mtu wa maana sana, ndio maana shetani anakutafuta kwa kila njia akumalize. Wewe ni mzalishaji kupitia wewe kuna vitu vikubwa vinazaliwa, kupitia wewe kuna mambo makubwa yatatokea katika ulimwengu. Yesu Kristo anapitia katika tumbo la mwanamke. Wewe ni njia nzuri ya kupitishia baraka. Hivi unajua hata katika familia kuna mambo mengi Mungu anayapitisha kupitia wewe? Funga milango ambayo shetani anaweza kuitumia kupenyeza vitu ambavyo si vya kiungu kwenye maisha yako. Funga milango inayoweza ondoa baraka za Mungu katika maisha yako. Usikubali shetani akutumie kufunga milango ya Baraka kwa maisha yako, kwa watoto wako, mume, ndugu taifa na kanisa.
Safari ya kuzaa huwa sio ya siku moja, mchakato wake huwa ni mrefu unahatua nyingi. Lakini kwa vile Mungu ameweka tumbo la uzazi ndani ya mwanamke basi kuzaa kutatokea tu, cha muhimu usiutupe mchakato. Kuitwa mama sio rahisi ila inawezekana kwasababu Mungu ameweka uwezo ndani yetu. Ameweka uwezo wa kuzaa na kuwa mama bora ndani ya nyumba mumeo akufurahie, watoto wakufurahie. Kuna wakati unafanya majukumu ya kuwa mama na hakuna anayetambua hiyo ni nafasi aliyokupa Mungu, ila tambua Mungu anakuona na anaitambua hiyo nafasi, pigana katika ulimwengu wa roho shetani asije akakufanya ukate tamaa. Kuna wakati maumivu uunayopitia yanakuwa makali sana, unakata tamaa, lakini usikate tamaa ipo siku mtoto atazaliwa, safari hii ni ndefu lakini iko siku kitu cha Ki-Mungu kitazaliwa, ipo siku utaona ndoto zikitimia katika maisha yako.
MWANAMKE NA UTUMISHI
That is about 62% of this chapter. The rest continues in the book.
Buy on Amazon ↗